Naibu Spika atoa ya moyoni

Kwa mara ya kwanza Naib Spika wa Bunge la Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Dk.Tulia Ackson amezungumzia shutuma dhidi yake za kutumiwa na Ikulu kuongoza Bunge


Kadhalika, Naibu Spika amezungumzia madai kutoka kwa baadhi ya watu kwamba alimshitaki Spika Job Ndugai kwa vigogo wa nchi.
 Dk. Tulia amesema kufuatia matukio yaliyotokea kwenye vikao vya Bunge lililopita ambalo wabunge kutoka vyama vinavyounda Umoja wa Katiba (Ukawa) walisusa.
Wabunge hao kutoka vyama vya Chadema, CUF na NCCR-Mageuzi pia waliwasilisha hoja wakitaka kung’olewa kwa Naibu Spika kwa kumtuhumu anatumiwa na Ikulu kuubana mhimili wa bunge na kuendesha vikao vyake kwa misingi ya kupendelea wabunge wa Chama cha Mapinduzi (CCM).
Dk. Tulia alizungumzia pia maoni ya Spika Ndugai juu ya sakata la mkataba wa Jeshi la Polisi na Kampuni ya Enterprises (Ltd) juu ya kufunga vifaa vya kuchukua alama za vidole kwenye vituo 108 nchini.
Katika taarifa hii iliyo kwenye mfumo wa maswali na majibu, Dk Tulia pia anazungumza kwa undani sakata lake na wabunge wanaotoka vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), waliosusia Bunge la bajeti kwa kutokuwa na imani na kiongozi huyo ambaye ni mwanasheria aliyebobea.
Swali: Vipi mahusiano yako ya kikazi na Spika, ni mazuri? Kwanini baadhi ya watu wanasema kuwa wewe unatumiwa na Ikulu kuendesha Bunge na wakati mwingine huwa unamshitaki Spika kwa Rais?
Jibu: Mahusiano yangu na Spika yako vizuri. Niseme tu kwamba Rais anateua wabunge 10 na anateua mawaziri na watu wengine, lakini hana mamlaka ya kuteua Spika na Naibu Spika, kwa hiyo watu wanasahau wanadhani kwamba unaibu Spika nimepewa sijui, nimeteuliwa na Rais, hapana, ubunge nimeteuliwa na Rais, unaibu spika nimechaguliwa na wabunge kama ambavyo angeweza kuchaguliwa yoyote aliyekuwa anagombea.
Kama nilivyokwambia tulikuwepo wawili tuliokuwa tunagombea, wote tulikuwa na sifa, lakini ikatokea mimi ndo niliyeshinda kwa asilimia 71.
Kwa hiyo watu wanadhani hii nafasi nimepewa na Rais, hapana, nimechaguliwa na kura za wabunge kwenye hii nafasi.
Lakini sasa mtu akisema napigiwa simu na Rais, hivi nchi hii kuna mtu ambaye hataki kupigiwa simu na Rais? Ama hapendi kupigiwa simu na Rais? Kwa sababu hata kama napigiwa ama sipigiwi, yeye anayenituhumu ana shida gani nalo hilo?
Ana tatizo gani? Ni sawa tu nikipigiwa na yeye kama mbunge, kwanini anapata tatizo kwamba napigiwa simu?.
Lakini tatizo ninaloliona ni kusema Naibu Spika, anapiga simu Ikulu kumsemea Spika, mimi namsemea Spika nimekuwa msemaji wake ama namsemea nini? Unajua kuna watu ni wazuri katika kuchonganisha watu, yeye kama anajua kwamba Spika huwa anasemewa, ameongea na Spika ndo akamwambia hivyo? Kwamba Naibu Spika huwa ananisema?
Kwa hiyo mimi nisingependa kwenda huko kwa sababu najua watu wengi tu wanatunga maneno, ni sawa na hili ulilosema kwamba Spika anapata taarifa za kuhusu madawati kwenye mtandao wa wa kijamii wa Watsapp (Sh. bilioni sita, ambazo Bunge lilipeleka kwa Rais ili zinunue madawati), nani alienda kumhoji Spika akamwambia kwamba amepata taarifa kwenye Watsapp? Anajua mimi nilitumwa na nani kwenda Ikulu?
Hajui lakini anajisema tu, sasa mimi sioni sababu ya kumtafuta kumjibu kumwambia unajua mimi nilitumwa na Spika kwenda Ikulu, siwezi kwenda huko kwa sababu naona tu ni mtu anatunga taarifa kwa sababu anataka kuziamini.
Kwa hiyo habari hizo za ugomvi ni watu wanatunga kwa sababu wanazojua wenyewe, lakini mimi huko nisingependa kwenda kwa sababu watu wanatunga mambo mengi, hilo ni mojawapo.
Swali: Ulichukuliaje uamuzi wa wabunge kusema hawana imani na wewe?
Jibu: Katika hali ya kawaida ukiwa kiongozi lazima ujifunze kuishi na watu wa kila aina, wakiwa pale ndani wakiwa kundi wakitoka ndo mtu unaona sijui wamefanyaje, lakini mimi ndiye ninayeshughulika na mambo yao ya kila siku ofisini pale.
Kwa hiyo yale nayowafanyia ofisini hawayakatai, hawasemi barua zao haziwezi kusainiwa na Naibu Spika na ruhusa wanaomba kwa Naibu Spika.
Kuna vitu wanafanya kwa jumla ni sawa (uamuzi wa wabunge wote wa Ukawa kutoka nje ya Bunge), ikija masuala yao ya mbunge mmoja mmoja, maombi sijui anapeleka wapi, hawezi sema maombi yangu sitaki yasomwe na Naibu Spika.
Lakini kwa sababu kama nilivyosema lile Bunge ni jumba la siasa, ni jambo jema tu wao kuonyesha msimamo wao lakini nadhani walichukua hatua nzuri tu kisheria na kikatiba, kwa maana ya kwamba walichukua hatua ambayo Katiba inatambua na kanuni zinatambua ya kupeleka hoja kwa Spika ya kutokuwa na imani na Naibu Spika.
Kwa hilo walifanya vyema kwa sababu katiba na kanuni inatambua kwamba waliokuchagua kuna wakati wakawa wamekuchoka ama hawakubaliani na namna wewe unavyowaendesha.
Kwa hiyo wewe umechaguliwa kwa kura watakuondoa walewale waliokuchagua, kwa sababu hiyo siyo jambo ambalo ningesema linanitisha ama limenitisha kwa wao kupeleka hoja kwa sababu ni jambo la kawaida katika uongozi.
Unaweza kuwepo pale ama ukaondolewa na wale waliokuchagua.
Lakini kutokutishwa huko kunatokana na kuelewa kwamba katiba imetaja, kanuni zimetaja, ni jambo linaloweza kutokea, lakini siwezi kusema kwamba kura zingetosha ama zisingetosha kwa sababu mimi nina kura moja tu.
Na walionipiogia kura kushika hiyo nafasi ni haohao wangeweza kuniondoa kwa hiyo siwezi kusema nina uhakika wasingeweza kuniondoa kwa sababu kura unayo moja, hayo ndio mazingira, lazima uwe tayari vinginevyo kama hujajiandaa, unaweza pata shinikizo la damu.
Swali: Ulikuwa unajisikiaje ukiona wabunge wa Ukawa wanavyotoka bungeni?
Jibu: Unajua ukiwa kiongozi lazima uone namna ambavyo jambo linalotakiwa kwisha lazima liishe, hili bunge halikuwa la kawaida kwamba unasema hoja hii tuiache tuimalize kesho, hoja ya bajeti ikiwa mbele hakuna hoja nyingine unaweza kuleta mbele.
Lingekuwa bunge jingine huenda mambo yangekuwa tofauti, kwa sababu hoja ya serikali lazima iishe, walivyokuwa wanatoka nilikuwa naona sawa, kwa sababu, sababu zao mimi binafsi sijazisikia kutoka kwao, ningezisikia kama hivi nimekaa na wewe hapa, ningesema sababu walizokuwa wanazitoa ni hizi.
Sasa sababu zao nimeziona tu kwenye vyombo vya habari, nisingeweza kuzisemea kwamba wao walikuwa na sababu gani haswa za kutoka.
Lakini katika uendeshaji wa Bunge na haswa mabunge mengine ya Jumuiya za Madola, kufanya walichofanya kama wangetoka mara moja ama mara mbili ama kutolewa siyo jambo la ajabu, wameshatolewa mara nyingi tu huko nyuma, jipya ni hilo la kutoka kila siku.
Ila sasa ukitoka unaowakilisha wanakosa mwakilishi, laiti ningejua sababu zinazowatoa ningejua kanuni fulani inalalamikiwa, ama kanuni fulani wanadhani nimevunja, badala ya kupeleka hoja kwa kamati wanaibeba wao wenyewe, sasa siwezi kwenda huko kwa sababu sijui wanacholalamikia.
Swali: Umewahi kuwaita kuzungumza nao?
Jibu: Unawaita kwa suala lipi? Labda hata wao wangeitwa waulizwe kwanini wanatoka ama waliwahi kuleta malalamiko yao rasmi, au kunifuata?
Swali: Vipi mahusiano yako na wabunge yako vizuri?
Jibu: Wabunge tena wote, hata hao wa upinzani, wakiwa kundi ndo wanatatizo kwamba wametoka pamoja, siyo kwamba mmoja mmoja hamuwasiliani ama hamuongei, hapana.
Swali: Kumekuwa na hoja kwamba umepewa nyadhifa nyingi kwa kasi, tunajua ulikuwa mhadhiri, ukawa Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali, ukachukua fomu kugombea uspika kabla hujateuliwa kuwa mbunge na ukagombea nafasi ya Naibu Spika ukaipata, hoja inakuja ni lini ulichukua kadi ya CCM?
Jibu: Hiyo ndo siasa moja kwa moja sasa naweza kusema, mtu anaweza kuona matatizo ya mtu mwingine, ama wanasema anaona boriti kwa mwenzie wakati yeye ana kibanzi.
Mimi sioni hizo ni kasi, ni hatua tu, kuwa Naibu Mwansheria Mkuu ni kuteuliwa na Ras, nilipoteuliwa kuwa wapo wanaojua na wengine hawakujua, hawakujua kama nafanya kazi ama nalala nyumbani, magazeti mengine yakawa yanaandika yanashangaa, sijui wao walitarajia nani ateuliwe.
Nikaja kuchukua fomu ya unaibu spika, wengine pia wakashangaa, wakaona huyu sijui ana matatizo gani, wakasema anatamaa na vitu kama hivyo lakini nisingekaa mahali kufikiria watu wanasemaje, wanafikiri nini? La msingi ni mimi kukaa na kuona nataka nini ndio nitakachofanya.
Sasa kusema kwamba kasi imewatisha watu na kusema sema, unajua mle bungeni kuna wabunge wa aina tano, wanaotoka kwenye majimbo, Baraza la Wawakilishi la Zanzibar, wanawake wanaoletwa na chama kulingana na kura (viti maalum), Mwanasheria Mkuu na sisi tulioteuliwa na Rais.
Kwa kundi la wanawake kwa kuwa ni mfumo wa vyama vingi kila chama kina utaratibu wake, tume (Tume ya Taifa ya Uchaguzi) wanataka majina, yanapatikana vipi ni kazi ya vyama, vyama vingine wanafanya kura za maoni, wanaoshinda wanaendelea, hao ni wa majimbo, wengine wa viti maalumu pia walifanya kampeni na zilizisikika, vyama vingine vilileta orodha majina ya watu ambao mpaka yanatangazwa na tume walikuwa na kadi za CCM.
Wao waliwapata wapi? Walichukua fomu saa ngapi za kujiunga na vyama vyao na kadi za zamani walirudisha lini? Hao ni wengi sihitaji kuwataja majina ndo maana nasema mtu ana kibanzi anaona boriti la mwenzake.
Kwa hiyo hoja ya mimi nilipata lini kadi ya CCM ni suala la chama changu kuliko mtu mwingine yoyote, kama chama kiliona naweza kugombea uspika wewe kwamba nilipata kadi lini una tatizo gani nalo?
Kama nilipata asubuhi kadi nikagombea mchana wewe linakuhusu nini? Kama chama changu kiliona ni sawa wewe una tatizo gani? Kwa sababu huo ni utaratibu wa chama changu, wewe chako pia kina utaratibu wake ambao hakuna anayekuuliza kwa hiyo ni mazingira kama hayo.
Nadhani tutafika mahali tuanze kujadili mambo ya msingi kuliko ambayo siyo ya msingi, hata hili la mimi nilichukua kadi lini sioni kama lina msingi.
Swali: Suala la wewe kuwa Naibu Spika ambaye hutokani na wabunge limekuwa likiibua maswali mengi, hali hiyo inatokana na nini?
Jibu: Ni kweli imezoeleka kwamba Naibu Spika anatokana na wabunge, lakini mambo mengi siku hizi yamebadilika, huko nyuma pia katiba ilikuwa inataka Spika ni lazima awe mbunge.
Ikaja ikabadilika, kwa hiyo sasa hivi mtu yoyote anaweza kuwa Spika, kikubwa tu apitie kwenye chama, lakini anaweza kuwa mtu yoyote, Naibu Spika ndiyo katiba inasema lazima awe Mbunge.
Kwa hiyo utagundua Naibu Spika anafanya kazi chini ya Spika, kama Spika anaweza kuwa mtu yoyote na na akaongoza vikao manake yeye ndo kiongozi wa mhimili.
Sasa kama kiongozi wa mhimili, katiba inatambua kwamba anaweza kuwa mtu yoyote, ilimradi awe na vigezo vya kuwa mbunge, mimi sioni kwa nini watu wanapata tabu na hili la Naibu Spika, kwa hiyo msingi ni huo, mabadiliko huwa yanachukua muda kuyazoea, mimi naamini tutafika kama jamii kuona zaidi mtu anafanya nini kuliko kuona mambo mengine kwa sababu yapo mengi ambayo watu wanaangalia unapokuwa kwenye nafasi.
Mtu ataangalia umri, ataangalia huyu ni mwanamke au mwanaume, akiwa mwanaume wanaona kwamba ni jambo la kawaida, akiwa mwanamke tayari mjadala utaanza, mwanamke kufanya kile lakini hakuna mwanaume atajadiliwa, kwa hiyo mimi naamini baada ya muda haya yote yatakaa vizuri badala ya kujadili mtu atajadili utendaji ama kazi anazofanya.
Swali: Kulikuwa na malalamiko kwamba, suala la Lugumi ulilifunika na likuwa halijaisha, hivi karibuni Spika kasema litarudi bungeni, maoni yako ni yapi juu ya namna ulivyolimaliza?
Jibu: Spika akishaongea mimi siwezi kufanya mjadala juu yake kwa sababu yeye ni kiongozi wangu. Kwa hiyo juu ya ninaonaje, haijalishi tena kwa sababu mkuu wangu keshaongea, kwa sasa haijalishi mimi naonaje.
Swali: Pia kumekuwa na malamiko kwamba ulimzunguka Spika ukarudisha fedha za Bunge kwa Rais (Sh bilioni sita) bila kumshirikisha, ukweli wa hili ukoje?
Jibu: Kwa kawaida kuna bajeti ambayo inatokana na maombi maalum, inapotokea jambo lililoombewa fedha limeisha, kuna utaratibu wake.
Kwa kawaida kama jambo limeisha yule alipelekewa fedha anaweza kumuomba waziri(Waziri wa Fedha) abadilishe matumizi ama kurudisha kabisa fedha kwamba hili jambo limeisha.
Fedha zile zilipatikana kupitia bajeti 2015/16, mwaka jana kulikuwa na uchaguzi kwa hiyo bunge lilivunjwa mapema, kwa hiyo wabunge walikuwa hawalipwi mshahara wala posho kwa hiyo fedha zilitokana na kubana matumizi kwenye maeneo mbalimbali na nyingine ndo zile.
Ofisa Masuhuri wa bunge ni Katibu wa Bunge, ndiye anajua fedha zilizoingia, kwa kutojua ndiyo wanadhani kuna chombo kinatakiwa kushirikishwa kabla ya kutoa fedha.
Mimi hata hizo akaunti za Bunge sizijui na sijui hata kama zina hela, yawezekana mtu hajui jambo lakini kwa sababu anajulikana na anajua akisema litaandikwa, basi anasema tu.
source:ipp media

No comments

Powered by Blogger.