Bavicha yakoleza Operesheni Ukuta
Baraza la vijana la chama cha demokrasia na maendeleo limetangaza kuunga mkono operesheni ya umoja wa kupambana na udikteta(UKUTA)ilio tangazwa hivi karibuni na kamati kuu ya chama hicho
Aidha, Bavicha wamemjibu Mkuu wa Mkoa wa Dar
es Salaam, Paul Makonda, kwamba hana mamlaka ya kuzuia operesheni hiyo
kwa kuwa wanaifanya kisheria na yeye siyo msajili wa vyama vya siasa.
Makonda aliagiza Jeshi la Polisi kuzuia
maandamano ya Ukuta, Ijumaa wakati akizungumza na Kikosi cha Kutuliza
Ghasia (FFU) katika kambi ya Ukonga.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar
es Salaam jana, Mwenyekiti wa Bavicha, Patrobas Katambi, alisema
maandalizi ya kuunga mkono operesheni hiyo yamekamilika kwa nchi nzima.
“Kauli ya Mkuu wa Mkoa (wa Dar es Salaam) ya
kusema kwamba polisi wahakikishe Ukuta haujengeki, haitekelezeki kwa
sababu yeye hana mamlaka ya kufanya hivyo na wala si msajili wa vyama
vya siasa hadi atoe kauli hiyo,” alisema Katambi.
“Zipo kesi nyingi zinazoonyesha wakuu wa mikoa
kufanya kazi ambazo haziwahusu, hivyo kauli yake tutaipima kisheria,”
alisema na kuongeza:
“Yeye akitaka aendelee kusema chochote
akijisikia, lakini sisi tunamwambia kwamba mikutano yetu iko pale pale
na tutaifanya nchi nzima.”
Katika mazungumzo yake na FFU, Makonda alisema
askari wanafahamu sheria, hivyo wasisubiri mtu yeyote kuja kuwakumbusha
juu ya jambo hilo.
Aidha, aliwataka polisi hao kutosubiri
maelekezo mengine kwa kuwa Amiri Jeshi Mkuu ambaye ni Rais John Magufuli
ameshaagiza kutofanyika kwa maandamano ya Ukuta yaliyopangwa kuwa
Septemba mosi.
Makonda aliliagiza jeshi hilo kuhakikisha
kwamba sheria zinafuatwa na kusiwapo kitu kinaitwa Ukuta ili wananchi
waendelee na kazi zao kama kawaida.
Lakini Mwenyekiti wa Bavicha jana alisema:
“Tunamtaka Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini (IGP), Ernest Mangu, ajiandae
kutuma jeshi lake kulinda mikutano yetu.”
Kuhusu onyo la Rais Magufuli aliloitoa akiwa
kwenye ziara ya kikazi mkoani Singida kwamba Chadema isimjaribu kwa
Ukuta, Katambi alisema chama hicho hakimjaribu.
Alisema Chadema itafanya maandamano nchi nzima
kwa sababu kwa njia hiyo wanamsaidia kutoa mawazo yao kama vyama vya
siasa kwa ajili ya kumsaidia kuendesha shughuli zake vizuri zaidi.
“Hatuna shida ya kumjaribu Rais, na wala si
kwamba tunamchukia, na wala hatuna sababu ya kupinga uwapo wake, na hata
ukiulizwa sasa kwamba Rais wako ni nani, lazima useme ni John
Magufuli,” alisema Katambi.
“Tunapotoa dosari na kasoro tunamsaidia kuendesha nchi yake na watu walio chini yake.”
“Sisi kama vyama vya siasa tuna haki, tunajua
yeye ndiye Rais, kama sisi hatukuweza kupata nafasi ya hiyo, haimaanishi
kwamba ni vita, isipokuwa kupitia vyama vyetu, tuna sehemu ya kutoa
mawazo yetu katika kuifanikishia serikali yake kuongoza vema pamoja na
watu wake wa chini tena kwa mujibu wa sheria na inamsaidia yeye kuwa
bora zaidi.
“Kwa hiyo kauli ya Rais sisi hatuna tatizo nayo.”
“Kwa hiyo kauli ya Rais sisi hatuna tatizo nayo.”
Katambi alisema taratibu zote za kisheria katika kutekeleza mikutano hiyo zitafuatwa.
Kamati Kuu ya chama hicho ilisema lengo la operesheni hiyo ni kuzuia matukio ya ukandamizaji wa haki na demokrasia nchini.
Leave a Comment